dc.description.abstract | Swahilihub ni tovuti iliyozinduliwa katika mwaka wa 2012 kwa lengo la kukuza Kiswahili
mtandaoni. Swahilihub ni miongoni mwa tovuti kuu za Kiswahili ambayo matumizi yake
yanazidi kuenea na kuimarika kwa sababu ya maendeleo ya kiteknolojia. Ujio wa mitandao
umebadili mikondo ya utangamano na kwa sasa majukwaa ya kidijitali ndiyo maeneo
makuu ya ukuzaji wa lugha. Kwa takriban mwongo mmoja, Swahilihub imekuwa
ikitumika katika sehemu mbalimbali za ulimwengu. Aidha, katika kipindi hiki, teknolojia
imekuwa kwa kasi kubwa mno na kuathiri Kiswahili. Licha ya maendeleo ya teknolojia
na athari zake, hakuna utafiti ambao umetathmini namna mradi wa Swahilihub unavyochangia
ukuzaji Kiswahili. Ni kutokana na msingi huu ambapo utafiti huu ulilenga kutathmini mradi wa
Swahilihub katika ukuzaji Kiswahili. Ili kulifikia lengo hili, utafiti huu ulikusudia kubaini
namna mfumo wa Swahilihub unavyochangia katika ukuzaji Kiswahili nchini Kenya,
kuchunguza matumizi ya Swahilihub katika ukuzaji Kiswahili, kupambanua changamoto
za matumizi yake pamoja na kujadili mikakati ya kuimarisha matumizi ya Swahilihub
katika ukuzaji Kiswahili nchini Kenya. Tathmini hii ilitumika kutoa mapendekezo ya mikakati
ya kuimarisha mfumo wa tovuti ya Swahilihub. Mwelekeo mseto wa utafiti unaohusu matumizi
ya mbinu za kimaelezo na kijarabati kwa pamoja ulitumika katika utafiti huu. Data ya utafiti huu
ilikusanywa kwa kutumia uchanganuzi wa matini mtandaoni, mahojiano nyanjani pamoja na hojaji
na mijadala miongoni mwa watumiaji wa Swahilihub katika baadhi ya vyuo vikuu nchini Kenya.
Utafiti huu ulitumia mahojiano kwa wasimamizi 5 wa Swahilihub na wahadhiri 15, huku hojaji ya
matumizi na ukuzaji Kiswahili pamoja na mijadala ya kimakundi ikitumiwa ili kubaini matumizi
na ukuzaji Kiswahili miongoni mwa watumiaji wake 320 katika vyuo vikuu nchini Kenya. Jumla
watafitiwa 340 walishiriki katika utafiti huu. Aidha utafiti huu ulitumia ARhefs na Similarweb
ambavyo ni vifaa vya tathmini ya tovuti ili kutathmini viwango vya ukubalifu na ustahilifu wa
Swahilihub miongoni mwa watumiaji wake. Data ya utafiti huu ilichanganuliwa kutokana na
malengo ya utafiti na kuongozwa na mihimili ya nadharia ya Msambao wa Uvumbuzi ya Rodgers
(2003). Matokeo ya utafiti huu yaliwasilishwa kwa njia za maelezo, majedwali, picha, michoro na
chati. Utafiti huu ulibaini kwamba viwango vya ukubalifu na ustahilifu wa Swahilihub vilikuwa
asilimia 45%. Aidha matokeo ya utafiti huu yalidhihirisha kwamba Swahilihub inastahimili
ushindani miongoni mwa tovuti zote mtandaoni kwa kiwango cha asilimia 0.13%. Matokeo ya
utafiti huu yalionyesha kwamba kulikuwa na changamoto anuai zilizokabili Swahilihub. Utafiti
huu pia ulijadili mustakabali wa Swahilihub katika ukuzaji wa lugha ya Kiswahili. Aidha utafiti
huu ulizua tasnifu kuwa utanuzi wa teknolojia pamoja na ustawi wa Swahilihub ni nafasi nzuri ya
uundaji wa dira ya ukuzaji endelevu wa lugha ya Kiswahili mtandaoni. | en_US |