Please use this identifier to cite or link to this item: http://ir-library.mmust.ac.ke:8080/xmlui/handle/123456789/2756
Title: TATHMINI YA MCHANGO WA SWAHILIHUB KATIKA UKUZAJI KISWAHILI NCHINI KENYA
Authors: OLOO, OWINO ANTHONEY
Keywords: MCHANGO WA SWAHILIHUB
UKUZAJI KISWAHILI NCHINI
KE
Issue Date: 2023
Abstract: Swahilihub ni tovuti iliyozinduliwa katika mwaka wa 2012 kwa lengo la kukuza Kiswahili mtandaoni. Swahilihub ni miongoni mwa tovuti kuu za Kiswahili ambayo matumizi yake yanazidi kuenea na kuimarika kwa sababu ya maendeleo ya kiteknolojia. Ujio wa mitandao umebadili mikondo ya utangamano na kwa sasa majukwaa ya kidijitali ndiyo maeneo makuu ya ukuzaji wa lugha. Kwa takriban mwongo mmoja, Swahilihub imekuwa ikitumika katika sehemu mbalimbali za ulimwengu. Aidha, katika kipindi hiki, teknolojia imekuwa kwa kasi kubwa mno na kuathiri Kiswahili. Licha ya maendeleo ya teknolojia na athari zake, hakuna utafiti ambao umetathmini namna mradi wa Swahilihub unavyochangia ukuzaji Kiswahili. Ni kutokana na msingi huu ambapo utafiti huu ulilenga kutathmini mradi wa Swahilihub katika ukuzaji Kiswahili. Ili kulifikia lengo hili, utafiti huu ulikusudia kubaini namna mfumo wa Swahilihub unavyochangia katika ukuzaji Kiswahili nchini Kenya, kuchunguza matumizi ya Swahilihub katika ukuzaji Kiswahili, kupambanua changamoto za matumizi yake pamoja na kujadili mikakati ya kuimarisha matumizi ya Swahilihub katika ukuzaji Kiswahili nchini Kenya. Tathmini hii ilitumika kutoa mapendekezo ya mikakati ya kuimarisha mfumo wa tovuti ya Swahilihub. Mwelekeo mseto wa utafiti unaohusu matumizi ya mbinu za kimaelezo na kijarabati kwa pamoja ulitumika katika utafiti huu. Data ya utafiti huu ilikusanywa kwa kutumia uchanganuzi wa matini mtandaoni, mahojiano nyanjani pamoja na hojaji na mijadala miongoni mwa watumiaji wa Swahilihub katika baadhi ya vyuo vikuu nchini Kenya. Utafiti huu ulitumia mahojiano kwa wasimamizi 5 wa Swahilihub na wahadhiri 15, huku hojaji ya matumizi na ukuzaji Kiswahili pamoja na mijadala ya kimakundi ikitumiwa ili kubaini matumizi na ukuzaji Kiswahili miongoni mwa watumiaji wake 320 katika vyuo vikuu nchini Kenya. Jumla watafitiwa 340 walishiriki katika utafiti huu. Aidha utafiti huu ulitumia ARhefs na Similarweb ambavyo ni vifaa vya tathmini ya tovuti ili kutathmini viwango vya ukubalifu na ustahilifu wa Swahilihub miongoni mwa watumiaji wake. Data ya utafiti huu ilichanganuliwa kutokana na malengo ya utafiti na kuongozwa na mihimili ya nadharia ya Msambao wa Uvumbuzi ya Rodgers (2003). Matokeo ya utafiti huu yaliwasilishwa kwa njia za maelezo, majedwali, picha, michoro na chati. Utafiti huu ulibaini kwamba viwango vya ukubalifu na ustahilifu wa Swahilihub vilikuwa asilimia 45%. Aidha matokeo ya utafiti huu yalidhihirisha kwamba Swahilihub inastahimili ushindani miongoni mwa tovuti zote mtandaoni kwa kiwango cha asilimia 0.13%. Matokeo ya utafiti huu yalionyesha kwamba kulikuwa na changamoto anuai zilizokabili Swahilihub. Utafiti huu pia ulijadili mustakabali wa Swahilihub katika ukuzaji wa lugha ya Kiswahili. Aidha utafiti huu ulizua tasnifu kuwa utanuzi wa teknolojia pamoja na ustawi wa Swahilihub ni nafasi nzuri ya uundaji wa dira ya ukuzaji endelevu wa lugha ya Kiswahili mtandaoni.
URI: http://ir-library.mmust.ac.ke:8080/xmlui/handle/123456789/2756
Appears in Collections:School of Education

Files in This Item:
File Description SizeFormat 
OWino Oloo.pdf7.78 MBAdobe PDFView/Open


Items in DSpace are protected by copyright, with all rights reserved, unless otherwise indicated.